Watangaza nia mnaitania Serikali au mko 'serious'?



"WATANGAZA NIA" MUNAITANIA SERIKALI AU MUKO "SIRIAZI"?


Kwa kipindi cha kama mwaka mmoja nimekua miongoni mwa watu wanaofuatilia kwa karibu kinachoendelea kuelekea uchaguzi mkuu wa wabunge na rais wa mwaka 2015. Kila nipatapo muda hujitahidi kumfualitia kila aliyeonesha nia ya kutaka kuwa kiongozi bila kujali ni udiwani, ubunge au urais. Ninawafuatilia kujua historia zao, kujua mawazo na mitizamo yao, kujua uwezo wao, kujua misimamo yao juu ya mambo ya msingi ya kitaifa na mengine mengi. Kwa kuwa hadi sasa wengi wa walionesha kwa uwazi kutaka uongozi wa nchi yetu hasa katika ngazi ya urais ni wanachama cha mapinduzi (CCM), nimekua makini zaidi kusikiliza kauli zao wanazozitoa kwa njia yoyote ile ili kuona wana mtazamo gani juu ya hali ya nchi yetu kwa sasa na wana mawazo gani mbadala ambayo wanadhani yataleta mabadiliko katika taifa letu.

Katika kuwasiliza wengi wa wanaotarajia kuteuliwa na chama chao kugombea nafasi ya urais, nimevutiwa na jambo moja kubwa ambalo ni utata au sintofahamu kati ya wanachokisifia kama mafanikio na wanachokiona kama matatizo wanayokusudia kuyatatua. Nimesema utata kwa sababu inakua ngumu kuelewa wanasifia nini, wanakosoa nini na wanataka kubadilisha nini. Ingawa kila mmoja amekua na mambo yake ambayo anayapa uzito wa kipekee, naweza kuweka mawazo yao katika ujumla bila kuwataja kwa majina kusema nani kasema nini. Ukiwasikiliza vema utaona kila mmoja wao anaonesha kwamba kuna mambo mengi hayajakaa sawa katika nchi. Utaona wanavyolalamika kuhusu ubovu wa mifumo iliyoko na kwa jinsi gani imeshindwa kukidhi mahitaji ya wakati na wananchi kwa ujumla wao. Baadhi ya malalamiko yao au mambo ambayo wanadhani yamekosa wa kuyatatua ni haya yafuatayo:
  • Nimewasikia baadhi yao wakionesha kwamba serikali na nchi inahitaji mabadiliko makubwa na kuna haja ya kufumua kila mfumo ulioko na kuweka mpya ikiwa ni pamoja na kubadili viongozi na watumishi ndani ya taasisi na idara za serikali kama namna ya kuleta tija
  • Nimewasikia karibu wote wakiongelea tatizo kubwa la ajira kwa vijana. Tatizo hili limepewa umuhim wa kipekee na wengine wameliona kama ajenda yao kubwa ya kutafuta nafasi ya kuteuliwa. Wanalalamika kwamba vijana wanasoma lakini hawana ajira na hawasikilizwi. Ingawa wengi wao ni sehemu ya serikali iliyoko nimewasikia wakionesha kwamba serikali imeshindwa kutatua tatizo hili
  • Nimewasikia wakielezea tatizo kubwa la rushwa katika nchi yetu. Wengi wa watarajiwa hawa wanalalamika kwamba nchi imeoza kwa rushwa na haki imepotea
  • Nimewasikiliza watarajiwa hawa wakieleza jinsi gani rasilimali za nchi hazitumiki vizuri kusaidia wananchi na kunufaisha taifa
  • Nimewasikia wakilalamika kwamba mfumo wetu wa elimu umeharibika na hauna mwelekeo na kiwango cha elimu yetu kimeshuka. Wanatuahidi kwamwba ndoto zao zikifanikiwa wataleta muharubaini wa elimu na kuifanya kuwa ya daraja la kwanza
  • Nimewasikia wakilalamika juu ya wizi wa mali za umma na ufisadi uliokithiri nchini
  • Nimewasikia wakiongelea kushuka kwa maadili na uminifu kwa watumishi wa umma 
  • Nimewasikia wakisema nchi imekua legelege na mambo yanachukuliwa ovyoovyo tu
  • Nimewasikia wakisema wanatamani wapewe nafasi wafanye maamuzi maana serikali iliyoko haifanyi maamuzi (magumu na mepesi) na hivyo kufanya mambo mengi kutotekelezeka
  • Nimewasikia wakiongela tatizo la huduma za kijamii kama maji, afya na usafiri. Wanaonesha ni kwa jinsi gani huduma hizi hazidhirishi na hakuna wa kuzitatua
  • Nimewasikia wakiongelea tatizo la uchumi na wana mawazo ambayo wanadhani yatabadilisha hali ya uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja

Sina tatizo na mambo haya iwapo waheshimiwa watarajiwa hawa wameyaona na wanadhani yanahitaji mtu sahihi kama wao kuyatafutia ufumbuzi. Tatizo langu liko katika mambo mawili:

Moja: ni ukweli kwamba watarajiwa hawa wote wako chama kinachoongoza serikali na wengi wao ni wajumbe wa vikao na mikutano ya maamuzi ya chama. Ninachojiuliza, haya mambo wamewahi kuyasema ndani ya chama chao? Mambo haya wamewahi kuyaelezea kwa mzigo na uzito huuhuu kwenye chama na serikali yao kama wanavyoonesha kwetu? Nini kilitokea?
  • Wengi wa watarajiwa hawa ni sehemu ya serikali na wenye nafasi kubwa ya maamuzi na kuleta mabadiliko. Haya wanayolalamika kuwa hayatendeki ndio hasa tuliyotegemea wayafanye kama majukumu yao ya msingi. Kwa nini hawayafanyii kazi sasa na wanadhani hadi wawe viongozi wakuu wa nchi ndio yatafanyika?
  • Labda na hili pia sio shida na huenda wana maelezo na sababu za msingi kwa nini mawazo na mipango yao haitekelezeki katika mazingira ya sasa ingawa ningetamani sana kujua sababu zao. Nijue walifanya nini kikawa kigumu kwao na kitakwendaje kuwa kirahisi baadaye.

Mbili: iwapo jambo la kwanza ni sahihi kwao au la, nina la pili linalonisumbua zaidi. Ukiwasikiliza watarajiwa hawa, utashangaa wanapokuwa katikati ya maelezo yao au mwishoni ghafla wanabadili kauli na kuanza kuisifia serikali iliyoko kwamba imefanya mengi na makubwa sana. Kama vile hiyo haina uzito wa kutosha, utawasikia wakimtaja Rais kwamba katenda mambo mengi sana makubwa na mazuri. Watamsifika kwamba kaipasiha nchi kimaendeleo na utendaji wake hauna mfano. Utawasikia wakisema pengo lake halitazibika na atakumbukwa daima.

Nini kunawakuta watarajiwa hawa? Kwa nini wanakua na kuali za kujichanganya? Inawezekanaje mtu ukuwa na malalamiko gunia nzima juu ya mambo ambayo unadhani yangefanywa na serikali au kusimamiwa na Rais aliyeko madarakani na wakati huohuo ukaanza kumsifia kwamba kafanya na anafanya mambo makubwa? Nini kinatokea? Huwa wanakumbuka kwamba bado hawajakabidhiwa bendera na kwamba kuna chama na kiongozi wake mkuu ambao wameshika mpini na wao wako kwenye makali?

Watarajiwa hawa huwa wanamaanisha nini? Kwa nini wasiwe wa kweli na wawazi tu katika yale wanayoyasimimia? Kwa nini wasiwe wazi tu kusema serikali na kiongozi wake wameshindwa kazi na ndio mana mambo yako jinsi yalivyo na hivyo wao wanakuja kubadilisha? Au kwa nini wasituambie tu kwamba serikali na Rais wetu wametenda miujiza na kuleta maendeleo makubwa na wao hawana jipya ila wanakwenda kusimamia tu yale ambayo kayafanya na kuendeleza mipango Rais anayoiacha?

Ninategemea wanapoanza kutangaza nia zao rasmi, watakumbuka kuliweka hili sawa na watupe kauli zisiyotukanganya, tututania wala kutudanganya. Zaidi sana wasimtanie Rais wetu na serikali yake. Tunaweza kuwaelewa tu na wanapotaka kutupeleka bila kumuhusisha yeye na serikali anayoiongoza.

Mwalimu MM
mmmwalimu@gmail.com

Post a Comment

Previous Post Next Post