HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA TAREHE 26 MEI, 2015 MJINI ARUSHA
Ndugu Gratian Mukoba, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, TUCTA;
Mhe. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Mheshimiwa Gaudencia Kabaka, Waziri wa Kazi na Ajira;
Mheshimiwa Celina Kombani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma;
Mheshimiwa Hamis Majaliwa, Naibu Waziri – TAMISEMI;
Mheshimiwa Margaret Sitta, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Jamii;
Mhe. Felix Daud Ntibenda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Ndugu Msulwa, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania;
Ndugu Nicholaus Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, (TUCTA);
Ndugu Ezekiel Oluoch, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania;
Ndugu Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Walimu Tanzania;
Mke wangu Mama Salma Kikwete;
Ndugu Walimu;
Wageni waalikwa;
Shukurani
Nakushukuru sana Rais wa Chama cha Waalimu Tanzania (CWT) Ndugu Gratian
Mukoba na viongozi wenzako wa CWT kwa kunialika na kunipa heshima kubwa
ya kufungua Mkutano wenu Mkuu. Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya
mkutano. Kufanikisha mkutano wa Wajumbe 1,200 si
kazi ndogo hata kidogo. Hivyo basi unapofanikiwa ni jambo linalostahili
pongezi. Hongereni sana. Pia nikushukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Arusha
na wananchi wote wa Mkoa huu kwa mapokezi mazuri na kwa kukubali kuwa
wenyeji wa mkutano huu. Mmekuwa wenyeji wema. Hongereni sana.
Pongezi kwa CWT
Ndugu Rais
Ndugu Waalimu;
Natoa pongezi kwa viongozi wa Chama cha Waalimu wanaomaliza muda wao kwa
kazi kubwa nzuri waliyofanya na kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana na
yanayoendelea kupatikana. Mmeifanya vyema kazi ya kutetea haki na
maslahi ya walimu. Tumejionea jengo kubwa na zuri la kitega uchumi
lililojengwa Ilala, Dar es Salaam. Jengo hili lijulikanalo kama Mwalimu House limependezesha
sana eneo la Ilala na jiji la Dar es Salaam. Kama kwamba hiyo haitoshi
hivi karibuni tumepokea habari nyingine njema za kuanzishwa kwa Benki
ya Waalimu itakayojulikana kama Mwalimu Bank. Mafanikio
haya na mengine mengi ambayo sikuyataja, yanafanya CWT kuwa moja ya
vyama vya wafanyakazi mahiri na makini nchini licha ya kuwa ndicho Chama
kikubwa kuliko chote chote. Hongereni sana viongozi na wanachama wa
CWT.
Risala ya Chama cha Waalimu
Ndugu Rais
Ndugu Waalimu;
Nimeisikia na kuipokea risala yenu nzuri mliyoiwasilisha kwangu muda
mfupi uliopita. Nawashukuru kwa risala yenu imeainisha mafanikio,
mliyopata, changamoto zinazowakabili na muhimu zaidi mmetoa ushauri
muafaka kuhusu namna bora ya kuzitatua. Ni risala inayotoa fursa ya
kujadiliana na kushirikiana na yenye lengo la kujenga na kuimarisha
mahusiano ya pande zetu mbili. Ni risala inayoonyesha kuwepo kwa
kushirikiana, kustahamiliana na kuaminiana kati ya walimu na Serikali
yao. Sisi sote inatupa funzo kuwa, pale panapokuwepo na uhusiano mzuri
na ushirikiano kati ya walimu na Serikali, haliharibiki jambo. Hata yale
mambo ambayo pengine yalionekana magumu, tumeweza kuyatatua kwa pamoja.
Hatuna budi kuendeleza hali hii ya mahusiano kati yetu siku zote.
Risala yenu pamoja na mambo mengine imeibua masuala tisa. Masuala
hayo ni kuhusu madaraja ya walimu; posho ya kufundishia; madeni ya
walimu; uhaba wa nyumba za walimu; utoaji wa elimu bora; mabadiliko ya
mafao ya pensheni; ukaguzi wa shule; Sekta ya Elimu katika BRN; na
mapungufu ya kiutendaji katika kuhudumia walimu. Mambo yote haya ni ya
msingi sana na yanastahili kupatiwa majawabu muafaka. Yapo ya kisheria,
ya kisera na ya kimfumo. Napenda kuwahakikishia kuwa nimeyapokea na
tutayafanyia kazi mambo yote kama kawaida yetu. Kama mlivyosema katika
risala yenu, baadhi ya mambo yanahitaji kukaa mezani kujadiliana na
kushauriana zaidi. Tutafanya hivyo. Nitajitahidi kwa yale yanayowezekana
niwe nimeyatatua kabla ya kumaliza muda wangu wa uongozi. Kwa yale
ambayo yanahitaji muda mrefu, nitahakikisha kuwa kabla ya kukabidhi
ofisi niwe nimeyawekea msingi mzuri ili iwe rahisi kwa Rais ajaye baada
yangu kuyakamilisha.
Hatua za Serikali Kushughulikia Madai ya Waalimu
Ndugu Rais na
Ndugu Waalimu;
Kwa uchache, nitapenda kuzungumzia hatua ambazo Serikali imechukua na
inazoendelea kuchukua kushughulikia madai ya waalimu. Kama
mlivyoainisha katika risala yenu, Serikali ninayoingoza imefanya
jitihada kubwa sana kupanua fursa za watoto wetu kupata elimu na sasa
tumeelekeza nguvu zetu katika kuboresha elimu inayotolewa. Kwa ajili
hiyo, tumeongeza shule za msingi kutoka 14, 257 mwaka 2005 hadi 16, 343 mwaka 2014, na kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka milioni 7.54 hadi milioni 8.23. Shule za Sekondari, zimeongezeka kutoka 1,745mwaka 2005 hadi 4,576 mwaka 2014 na kuongeza wanafunzi kutoka 524, 325 hadi milioni 1.8 kati ya mwaka 2005 na 2015. Hali kadhalika, idadi ya vyuo vikuu imeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi 52 mwaka 2015, na kufanya idadi ya wanafunzi kuongezeka kutoka 40, 719 hadi200, 986 katika kipindi hiko.
Sote tunafahamu kuwa shule na elimu haikamiliki pasipo na waalimu na
pasipokuwa vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Upanuzi huo
mkubwa ulilazimu kupanua vyuo vya ualimu. Idadi ya vyuo vya ualimu vya
cheti na stashahada vimeongezeka kutoka 52 mwaka 2005 hadi 126mwaka 2015. Upanuzi huu ukiongeza na ule wa vyuo vikuu umewezesha kuongeza idadi ya waalimu wa msingi na sekondari kutoka 153, 767mwaka 2005 hadi 301,960 mwaka
2015. Hii imewezekana kutokana pia na uamuzi wetu wa kutoa mikopo kwa
wanafunzi waliochagua kusomea ualimu, na kuwahakikishia ajira pale
wanapomaliza masomo yao.
Serikali imefanya jitihada pia za kuboresha maslahi ya waalimu kadri
uwezo uliporuhusu. Hatukuweza kutoa nyongeza kubwa kwa wakati mmoja
lakini tumeongeza mara kwa mara. Kati ya 2005 – 2015 kumekuwepo na
ongezeko la kianzio cha mshahara cha Mwalimu mwenye cheti, Mwalimu
mwenye Stashahada ya Ualimu na wale wenye elimu ya shahada. Watumishi
wa kada nyingine za Serikali wenye elimu ya viwango hivyo, huanza na
mshahara wa chini ya ule wa waalimu. Nafahamu kuwa kiwango hiki bado
hakitoshi, lakini ukweli ni kuwa hakuna upungufu wa dhamira kwa upande
wa serikali, ila kikwazo ni kutokuwepo na uwezo mkubwa kimapato kwa
upande wa Serikali. Ukizingatia kuwa walimu ni asilimia 52.7 ya
watumishi wa Serikali, hivyo, ongezeko katika mshahara wa waalimu
linaleta mabadiliko makubwa sana katika bajeti ya Serikali. Kwa ajili
hiyo hatukuweza kutoa nyongeza kubwa kwa wakati mmoja lakini tumeongeza
mara kwa mara mpaka tumefikia hapa tulipo leo. Na katika bajeti hii
tutaongeza tena. Hivyo nitawaacha mahali penye unafuu ukilinganisha na
tulikotoka.
Tumeendelea pia kushughulikia kero nyingine za waalimu ikiwemo madeni na
madai yenu. Deni la waalimu lililopokelewa lilikuwa shilingi bilioni 53, 185,440,406 lililohusu waalimu 70,668. Baada ya uhakiki uliofanyika kwa kuhusisha Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali, jumla ya shilingi bilioni 23, 233, 654, 025 zililipwa kwa waalimu 29,243. Serikali imeshatoa ahadi ya kulipa ifikapo mwezi Agosti mwaka huu madai mengine ya waalimu 7,169 yenye jumla ya shilingi bilioni 9, 285,283,600 ambayo uhakiki wake umekamilika. Aidha, madai ya walimu 30,807yenye jumla ya shilingi bilioni 17,346, 593, 468 hayakuweza
kulipwa kutokana na kukutwa na dosari za msingi za kihasibu na
kiutaratibu. Wametakiwa kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Jambo la kururahisha katika ukaguzi na uhakiki huo wa madeni ni kule
kushirikishwa kwa Chama cha Walimu. Kwa pamoja tumethibitisha palipokuwa
sahihi na pasipokuwa sahihi. Inasikitisha kupata taarifa za kuwepo
vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Serikali
na walimu vinavyochangia kuzalisha madeni bandia. Vitendo vyao hivyo
ndivyo vinavyofanya madai yachukue muda mrefu kulipwa kwa kulazimika
kuweko na uhakiki wa ziada. Naungana nanyi katika pendekezo lenu la
kutaka watumishi hawa kuwajibishwa, maana ndio mzizi wa fitna kati ya
waalimu na Serikali. Nimekwishaeleza mamlaka husika kufanya hivyo bila
ajizi.
Ndugu Rais na
Ndugu Waalimu;
Tumeshughulikia lile dai kubwa la waalimu la marekebisho ya
muundo wa utumishi wa waalimu (Teacher’s Service Scheme). Tumepitisha
Muundo mpya wa Waalimu ambao umeanza kutumika toka Julai 1, 2014.
Nimesikia kuwa utekelezaji wake haukuweza kuanza kote nchini mara moja,
napenda kuwahakikishia kuwa katika mwaka ujao wa fedha tutahakikisha
kuwa Waalimu wote watakuwa wamefikiwa. Sambamba na hili la Muundo,
tumekwishapeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume ya Utumishi
wa Waalimu (Teachers Service Commission) ambao tayari umesomwa kwa mara
ya kwanza. Mawasiliano yanaendelea na Ofisi ya Spika ili Muswada huo
ujadiliwe katika Bunge hili la Bajeti. Tunafanya hivyo pia kwa Muswada
wa kuanzisha Bodi ya Taifa ya Taaluma ya Waalimu (Teachers Proffessional
Board). Nimepokea maoni yenu ya kutaka uangaliwe uwezekano wa Bodi hii
kuwa sehemu ya Tume ya Utumishi wa Waalimu badala ya kuwa na vyombo
viwili tofauti. Hoja yenu ya kutaka kupunguza utitiri wa vyombo
vinavyoshughulikia maslahi ya waalimu ina mashiko. Ushauri wenu
umepokelewa, tutautafakari na kuufanyia kazi.
Napenda kuwahakikishia kuwa madai yenu mengine ikiwemo nyumba
za waalimu, motisha kwa waalimu, mazingira ya kufanyia kazi, mafunzo
vikokotoo vipya vya pensheni na masuala mengine mliyoibua katika risala
yenu tutayashughulikia na tutawapeni taarifa. Pia nitaelekeza mamlaka
zinazohusika kukutana na uongozi mpya wa Chama chenu baada ya uchaguzi
mkuu wenu kuyajadili masuala hayo na kuyatafutia majawabu.
Napenda kusisitiza kwenu kwamba mimi na wenzangu Serikalini
tunawathamini sana na kuwapenda waalimu kwa dhati ya mioyo yetu. Sisi
tunatambua nafasi ya Mwalimu katika maendelo ya mtu binafsi na taifa kwa
jumla. Hakuna badala yake. Hivyo basi tunatambua wajibu wetu wa
kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Tumefanya jitihada
kutimiza wajibu wetu. Pale panapojitokeza matatizo yoyote si makusudio
yetu. Kitendo cha makusudi na anapojulikana mtu huyo atawajibishwa
ipasavyo. Wakati mwingine matatizo yanayowakuta hutokana na watu wetu
kuelemewa na mzigo kutokana na ukubwa wa kada yenu katika utumishi wa
umma ambapo ni asilimia 52. 7.
Kwa ukubwa huu, mnaweza kuelewa ni changamoto kiasi gani zinazojitokeza
katika kushughulikia masuala yenu. Ndio sababu hatuchoki kutafuta muundo
bora wa kushughulikia matatizo yenu. Ninachoomba kutoka kwenu ni
uvumilivu na uelewa wenu na kuwaomba mtupime kwa dhamira yetu na utayari
wetu wa kuyashughulikia madai yenu na si kwa idadi ya changamoto
zinazojitokeza.
Uchaguzi Mkuu wa CWT
Ndugu Rais na
Ndugu Waalimu;
Moja ya Agenda kubwa ya Mkutano wa leo ni Uchaguzi Mkuu.
Nitumie fursa hii kuwapongeza viongozi mliochaguliwa katika ngazi ya
Tawi, Wilaya na Mkoa ambao kwa pamoja mmeunda Mkutano Mkuu huu.
Nawapongeza kwa kuuendesha uchaguzi wa ngazi za chini vizuri maana
natambua kuwa haikuwa kazi ndogo kutokana na ukubwa wa nchi yetu, na
hamasa ya waalimu kisiasa.
Nawapongeza sana viongozi wote waliojitokeza kugombea nafasi
za uongozi wa ngazi ya Taifa. Naamini nyote mnatosha kwa nafasi
mnazoomba. Naomba mkumbuke kuwa si kila mtu aliyeomba atashinda.
Nafasi si nyingi kiasi hicho. Hivyo basi, wale ambao kura hazitatosha
safari hii, watumie uzoefu walioupata katika uchaguzi huu kujinoa zaidi
kwa chaguzi za miaka ijayo. Haitakuwa vizuri iwapo wale ambao
hawatafanikiwa kushinda, wataendeleza nongwa na kuwa chanzo cha kuvunja
mshikamano mzuri mlionao katika Chama cha Walimu. Kama nilivyosema
awali, sisi sote tunawaangalia waalimu kama kioo cha maadili na upevu
katika jamii yetu. Naamini hamtatuangusha.
Nawapongeza na kuwashukuru sana viongozi wanaomaliza muda wao
kwa ushirikiano wenu mkubwa mliotupatia sisi katika Serikali katika
kipindi chenu cha uongozi. Kwa pamoja tumeweza kutatua changamoto nyingi
za waalimu na kujenga madaraja kati yetu yaliyozaa mahusiano mazuri
ambayo ndio msingi wa kutatua madai ya waalimu kila yalipojitokeza. Ni
matumaini yetu kuwa viongozi watakaochaguliwa, wataendeleza pale
mlipoishia na muhimu zaidi uhusiano mzuri na ushirikiano na Serikali.
Sisi tunaahidi kuwapa kila aina ya ushirikiano unaostahili. Ni jambo
lenye maslahi kwetu sote.
Hitimisho
Ndugu Rais na
Ndugu Waalimu;
Hii ni fursa yangu ya mwisho kukutana na kuzungumza na
viongozi wa CWT nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya
hapo nitakuja kumsindikiza Mwalimu mwenzenu akija mkutanoni. Hivyo,
sina budi kutumia fursa hii pia kuagana nanyi na kupitia kwenu kuagana
na Waalimu wote nchini. Nirudie tena kuwashukuru sana kwa mchango wenu
mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini. Kwa kweli mnajitoa sana na
mnafanya kazi kubwa ambayo inaonekana na wote. Napenda kuwatia moyo kuwa
msilegeze uzi bali muendelee na moyo na wito wenu huo. Nitawakumbuka
sana waalimu katika maisha yangu baada ya kustaafu uongozi, kwa msaada
wenu na ushirikiano wenu. Nimewapenda, ninawapenda na nitaendelea
kuwapenda ‘Shemeji’ zangu.
Nawatakia Uchaguzi Mkuu na Mkutano Mkuu mwema.
Akhsanteni kwa kunisikiliza