Mtoto wa miaka tisa wa darasa la tatu Edrina Mafwele ameuawa kwa kunyongwa nyumbani kwao eneo la 'Kola Hill' Mkoani Morogoro.
Akizungumzia
tukio hilo, baba wa mtoto huyo, Barnabas Mafwele amesema awali marehemu
huyo aliwahi kukabwa na mtu aliyeficha uso wake kwa mavazi maarufu ya Kininja,
akiwa nyumbani kwao wiki kadhaa zilizopita, ambapo marehemu alihisi
tukio hilo lilitendwa na mtoto wa ndugu yao waliyekuwa wakiishi naye.
Amesema
kutokana na mazingira hayo, kabla ya tukio la kuuawa kwa mtoto wake
nyumbani kwao, walikuwa wamebaki yeye na ndugu yake huyo anayeitwa
Judith Jumile, mwenye umri wa miaka 15 anayesoma kidato cha kwanza
katika shule ya sekondari Kola Hill, ambaye anashikiliwa na Polisi kwa
tuhuma za kumnyonga hadi kufa marehemu Edrina Mafwele.
Akizungumza
kwa masikitiko kuhusu tukio hilo, Mwalimu wa marehemu kutoka ya Shule
ya Msingi Bernard Benderi, Twamba Benedict amesema marehemu alikuwa
mtoto mwema na mcheshi, huku wanafunzi wa shule aliyokuwa akisoma
mtuhumiwa wa mauaji hayo wakisema wamekuwa na wasiwasi na mwenendo wa
mwanafunzi mwenzao kutokana na tabia zake za ugomvi wa mara kwa mara.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paulo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza uchunguzi zaidi unaendelea.