Wanaotunga na kusambaza ujumbe kupitia SMS waonywa


Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini ADVERA BULIMBA
Jeshi la polisi nchini limetoa onyo kwa baadhi ya watu ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakitunga na kusambaza ujumbe kupitia simu za mikononi na mitandao mbalimbali ya kijamii wenye lengo la kuwatia hofu wananchi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Jeshi hilo limesema kuwa, watu hao wanaosambaza taarifa hizo wanajifanya kwamba taarifa hizo zimetoka kwenye taasisi za kimataifa na taasisi zingine zinazoaminika jambo ambalo siyo kweli.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na msemaji wa Jeshi hilo ADVERA BULIMBA linawataka wote wenye tabia hiyo kuacha mara moja na badala yake, endapo mtu yeyote anayo taarifa ya uhalifu wa aina yoyote ama kikundi chochote cha uhalifu atoe taarifa hiyo katika kituo chochote cha Polisi au kupitia simu za makamanda wa polisi wa mikoa ama vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili taarifa hizo ziweze kufanyiwa kazi haraka.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa taarifa zote zinazopokelewa ili kuhakikisha kwamba usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kusambaza ujumbe wenye mlengo wa upotoshaji, uchochezi ama kuwatia hofu wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post