

VIFO mfululizo vya wasanii wa 'Bongo Movies Unity' vilivyotokea mwezi uliopita vimeitikisa kampuni ya 5 Effects Movies Ltd hali iliyosababisha waweke ratiba ya kufanya ibada ya maombi kila siku kabla ya kuanza kazi zao, huku kila mmoja akimwomba msamaha mwenzake kwa mambo aliyomkosea.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, William Mtitu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Bongo Movies Unity alisema kuwa ameamua kufikia uamuzi huo baada ya kutambua kwamba kifo kinaweza kumpata mtu yeyote bila hata kuugua na kukosa muda wa kutubu kama ilivyowatokea wasanii hao wenzao.
"Siyo siri vifo vya wasanii wenzetu Adam Kuambiana, Rachel Haule 'Recho' na George Tyson vimenifanya niweke utaratibu wa kufanya maombi kabla na baada ya kufanya kazi, ili kujikabidhi mbele za Mungu hiyo ikiwa ni pamoja na kuomba toba kwa sababu hakuna ajuaye baadaye yake kama ilivyowatokea wasanii wenzetu," alisema Mtitu.
Aidha, Mtitu alisema mbali na kusameheana wafanyakazi wao kwa wao pia wanajitahidi kuwaomba msamaha watu waliowakosea japo ni ngumu, lakini hakuna namna, kwani lengo lao ni kujiweka tayari wakati wowote hata kama ikitokea mmoja wao akafa ghafla afe akiwa msafi na kuingia peponi moja kwa moja.
Katika hatua nyingine Mtitu alisema kuwa wapo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha filamu ya 'Stupid Father' ambayo marehemu Kuambiana alicheza na itakamilika mwezi huu na kuiingiza sokoni, kwani baada ya sinema ya Mr.Kamadana aliyoicheza kwa ustadi mkubwa ilifanya vizuri.